Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
ULEGA: TUMEJIPANGA KUIMARISHA BIASHARA YA MAZAO YA MIFUGO
10 May, 2024
ULEGA: TUMEJIPANGA KUIMARISHA BIASHARA YA MAZAO YA MIFUGO

 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema wizara yake imejipanga kuyasimamia vyema mazao ya mifugo hususani maziwa, nyama na ngozi ili yazalishwe kwa ubora na kushamirisha biashara kwa lengo la kuyafanya mazao hayo kuwa na mchango mkubwa zaidi kwenye pato la Taifa.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya Nyama na Bodi ya Maziwa kwenye kikao kilichofanyika jijini Dodoma Mei 7, 2024, ambapo alipokea taarifa za utekelezaji wa bodi hizo ambazo kwa sasa zimeunganishwa na kuundwa taasisi moja itakayosimamia mazao hayo ya mifugo.

“Tuko katika uundaji wa Taasisi nyingine ya usimamizi wa mazao kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, tunakwenda kuunda taasisi nzuri, makini, imara, itakayokwenda kuongeza tija na kushamirisha biashara. Wadau msiwe na wasiwasi, tunatambua juhudi kubwa mnazozifanya, tumejipanga kufanya kazi kwa pamoja kuleta maendeleo ya Tasnia hizi mbili na Sekta ya Mifugo kwa ujumla”, alisema 

“Niwaahidi kuwa tutajitahidi kwa upande wetu kama serikali kuyasimamia mazao haya, kuhakikisha biashara zinakuwa rasmi, na kuchangia zaidi kwa uchumi, lishe, na ajira”, aliongeza

Aidha, alitumia nafasi hiyo pia kuwaomba wananchi kuendelea kunywa maziwa na kula nyama kwa wingi kwani kwa  kufanya hivyo watachangia kuinua tasnia za maziwa na nyama na kukuza uchumi wa Taifa. 

Katika hatua nyingine, Waziri Ulega  amewahimiza Wafugaji kuzalisha zaidi maziwa na nyama zenye ubora kwani bado mahitaji ya bidhaa hizo ni makubwa ndani na nje ya nchi.