UNYWAJI WA MAZIWA SHULENI WATAJWA KUIMARISHA AFYA NA UFAULU KWA WANAFUNZI

KATIBU Tawala Mkoa wa Geita, Mohammed Gombati, amesema kuwa unywaji wa maziwa safi na salama kwa wanafunzi shuleni ni msingi wa afya bora na ufaulu wa wanafunzi katika Mkoa wa Geita.
Gombati aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Wadau wa Tasnia ya Maziwa leo septemba 23,2025 lililofanyika katika Ukumbi wa Nyerere uliopo katika Viwanja vya Maonesho ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mkoani Geita.
Akizungumza katika kongamano hilo lililoongozwa na kauli mbiu isemayo ‘Kwa Matokeo Mazuri Shuleni na Afya Bora, Maziwa Ndio Mpango Mzima,Katibu Tawala huyo alisisitiza kuwa viongozi wa shule, walimu, wazazi na walezi wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanafunzi wanapata maziwa wakiwa shuleni, huku akihimiza kuwa zoezi hilo liwe endelevu ili kukabiliana na changamoto ya udumavu wa mwili na akili miongoni mwa watoto.
Aidha, amewataka maafisa lishe katika mkoa huo kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora na matumizi ya maziwa safi na salama, kwa lengo la kuinua hali ya afya kwa watoto na jamii kwa ujumla.
Vilevile, ameagiza maafisa mifugo kuendelea kuwahamasisha wafugaji kufuga kisasa ili kuhakikisha upatikanaji wa maziwa ya kutosha kwa kipindi chote cha mwaka.
“Ni muhimu kuhakikisha kuwa mpango huu wa unywaji wa maziwa mashuleni unakuwa wa kudumu, na unaleta matokeo chanya katika maendeleo ya elimu na afya kwa wanafunzi wetu,” amesema Gombati.
Ametoa wito kwa washiriki wa kongamano hilo kutoa maoni yatakayosaidia kuunda mpango bora na wenye tija kwa Taifa, hususan katika sekta ya maziwa na lishe mashuleni.
Kwa upande wake, Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Bi. Deorinidei Mng’ong’o, amesema kuwa kongamano hilo linatarajiwa kujadili na kuweka mikakati ya utekelezaji wa mpango mahsusi na endelevu wa kuhakikisha wanafunzi wanapata maziwa shuleni ili kukuza afya ya mwili na akili.