UZALISHAJI WA MAZIWA NCHINI WAPANDA

Uzalishaji wa Maziwa Nchini umeongezeka kutoka lita bilioni 3.97 kwa mwaka 2023/2024 mpaka kufikia lita bilioni 4.01 kwa mwaka 2024/2025.
Hayo yamesemwa Juni Mosi 2025 Mkoani Morogoro na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Dkt. Ashatu Kijaji Katika siku ya kilele Cha Maadhimisho ya wiki ya Maziwa kitaifa ambapo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji alioufanya katika sekta ya mifugo na kwamba Uwekezaji huo umewezesha Tasnia ya Maziwa kuongeza mchango wake kwa asilimia 2 katika Pato la Taifa na kukua kwa asilimia 2.3 kwa mwaka.
Kuhusu mafanikio katika uzalishaji, ukusanyaji na usindikaji wa maziwa Dkt. Kijaji amesema kuwa yamepelekea matumizi ya maziwa na bidhaa zake kuongezeka kufikia wastani wa lita 68.1 kwa mwaka na kuipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bodi ya Maziwa Tanzania na wadau wa Sekta kwa kufanya kazi kubwa katika kuendeleza Tasnia ya Maziwa nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kigoma Malima ameahidi Morogoro kuwa Mkoa wa mabadiliko ya sekta ya mifugo Tanzania na kuiomba wizara isaidie kuongeza uzalishaji wa nyama na maziwa.
Awali Msajili wa Bodi ya Maziwa Prof. George Msalya amesema kuwa Kaya elfu nne zenye wastani wa watu elfu ishirini zinategemea uzalishaji wa maziwa kwenye uchumi wake ambapo jumla yauwekezaji wa Tirioni 3.2 na ajira elfu 3 zinategemea uzalishaji huo.