Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
WATAALAM WAONYA HATARI YA MASALIA YA DAWA KWENYE MAZIWA, WADAU WAPEWA MAFUNZO MBEYA
19 May, 2026
WATAALAM WAONYA HATARI YA MASALIA YA DAWA KWENYE MAZIWA, WADAU WAPEWA MAFUNZO MBEYA

Wataalam wa Tasnia ya Maziwa nchini wameonya juu ya matumizi holela ya dawa kwa mifugo ambayo husababisha uwepo wa masalia ya dawa katika maziwa, hali inayoweza kuhatarisha afya za walaji na kuathiri ubora wa bidhaa za maziwa. 

Onyo hilo limetolewa wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa Tasnia ya Maziwa kuhusu magonjwa yanayoambukizwa kati ya wanyama na binadamu pamoja na usalama wa maziwa yanayofanyika katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) Mei 19, 2026.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Uchumi na Uzalishaji wa Mkoa wa Mbeya, Afisa Mifugo wa Mkoa, Bw. Adam Mhagama, alisema kuwa sekta ya maziwa ina mchango mkubwa katika afya, lishe na uchumi wa wananchi, hivyo ni muhimu kwa wadau wote kuzingatia usalama wa maziwa kuanzia shambani hadi kwa mlaji wa mwisho. 

Alisisitiza kuwa elimu hiyo itasaidia kupunguza hatari ya magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na kuongeza imani ya walaji kwa bidhaa za maziwa zinazozalishwa nchini.

Kwa upande wake, Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, Prof. Hezron Nonga, alisema matumizi holela ya dawa kwa mifugo yanaweza kusababisha uwepo wa masalia ya dawa katika maziwa, jambo linaloweza kuhatarisha afya ya walaji na kuathiri ubora wa bidhaa za maziwa. 

Alifafanua kuwa kupitia mafunzo hayo, wadau wanaelimishwa juu ya matumizi sahihi ya dawa, muda wa kusubiri kabla ya kuuza maziwa baada ya matibabu ya mifugo pamoja na mbinu bora za usafi na uhifadhi wa maziwa.

Naye Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Prof. George Msalya, alisema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali na wadau kuhakikisha Tasnia ya Maziwa nchini inakuwa salama, yenye ushindani na inayochangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa taifa. 

Aliongeza kuwa elimu kuhusu dhana ya Afya Moja (One Health) ni muhimu katika kuunganisha afya ya binadamu, mifugo na mazingira ili kukabiliana na changamoto za kiafya zinazoweza kuathiri jamii.

Prof. Msalya pia aliwataka wadau wa Tasnia ya Maziwa kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uzalishaji wa maziwa salama huku akihimiza matumizi ya teknolojia bora na ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za Serikali, wataalam na wafugaji katika kuimarisha Tasnia hiyo.

Akizungumza mara baada ya mafunzo hayo, mmoja wa washiriki na mdau wa Tasnia ya Maziwa mkoani Mbeya alisema mafunzo hayo yataongeza uelewa kuhusu udhibiti wa magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, kuboresha afya za walaji, kuongeza imani ya soko kwa bidhaa za maziwa pamoja na kuongeza kipato kwa wadau wa Tasnia hiyo kupitia uzalishaji wenye kuzingatia viwango vya kitaalamu.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza uwezo wa wadau katika kudhibiti magonjwa, kuimarisha ubora wa maziwa na kulinda afya za walaji, hatua itakayosaidia kukuza Tasnia ya Maziwa na kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.