Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
WANAFUNZI ZAIDI YA 3,000 WAFIKIWA WIKI YA MAZIWA MOROGORO
24 Jun, 2025
WANAFUNZI ZAIDI YA 3,000 WAFIKIWA WIKI YA MAZIWA MOROGORO

Katika kuhamasisha Unywaji wa Maziwa kwa jamii,  Bodi ya Maziwa Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maziwa hapa nchini imehamasisha unywaji maziwa kwa wanafunzi zaidi ya 3,000 wa shule mbalimbali za Msingi na Sekondari wakati wa Maadhimisho ya 28 ya Unywaji Maziwa yaliyofanyika hivi karibuni Mkoani Morogoro.

Akiongea kwa nyakati tofauti wakati wa zoezi la uhamasishaji wa unywaji wa maziwa kwa wanafunzi Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania Prof. George Msalya amewataka Wanafunzi kupendelea kutumia maziwa na bidhaa zake kwakuwa kuna virutubishi muhimu kwa ajili ya ukuaji ukizingatia kuwa bado wako katika hatua za ukuaji wa kimwili na kiakili hivyo yatawasaidia kuliko kutumia bidhaa nyingine ambazo hazina manufaa kwao.

‘Niwasihi wanafunzi kuendelea kutumia maziwa hasa yaliyosindikwa licha yakuwa hutumika kama kiburudisho lakini ni lishe nzuri pia huongeza akili kwa watoto’ Amesisitiza Prof. Msalya

Naye Afisa Lishe kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia akiongea wakati wa uhamasishaji huo amewasisitizia wanafunzi kutumia maziwa kwani ni muhimu kwa ajili ya afya, hivyo amewataka kwenda kuwaeleza wazazi wao umuhimu wa kutumia maziwa badala ya viburudisho vingine.

Afisa Masoko kutoka Bodi ya Maziwa Tanzania Bw. Hamis Kiimbi amesema kuwa mpaka sasa shule nyingi nchini zimehamasika kuendesha mpango wa unywaji maziwa shuleni ukilinganisha na miaka mitano iliyopita hali iliyopelekea kuongezeka kwa ufaulu kwa wanafunzi pamoja na kuchochea mahudhurio kwa watoto wa shule.

‘Shule nyingi zinazotekeleza Mpango wa Maziwa Shuleni umedhihirisha kwamba watoto wakipata maziwa shuleni huchochea mahudhurio makubwa kwa wanafunzi hali inayopelekea kupungua kwa wanafunzi watoro na wanaoacha shule bila sababu hivyo kuongeza ufaulu kwa wanafunzi’ Amesema Kiimbi

Bodi ya Maziwa Tanzania katika Maadhimisho yake ya 28 ya Wiki ya Maziwa Kitaifa yaliyofanyika Mkoani Morogoro imefanikiwa kutembelea shule za Msingi Kiwanja Cha Ndege, Agape, Mwembesongo na shule ya Sekondari Kitungwa ambapo wanafunzi zaidi ya 3,000 walikunywa lita 2340 za maziwa.