Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
WATAKIWA KUHAKIKISHA MAZIWA YANAZALISHWA KWENYE MAZINGIRA BORA
29 May, 2025
WATAKIWA KUHAKIKISHA MAZIWA YANAZALISHWA KWENYE MAZINGIRA BORA

Naibu katibu mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi Sospeter Mtwale amewataka maafisa ugani walioteuliwa kwa sheria ya maziwa kuwa wakaguzi wa maziwa kwenye mamlaka za Serikali za mitaa na kutekeleza majukumu yao ya kuhimiza maendeleo ya tasnia ya maziwa na kuhakikisha maziwa yanazalishwa kwenye mazingira bora na kuchangia Pato la Taifa.

Alisema hayo kwenye maadhimisho ya wiki ya maziwa ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Morogoro ambayo yameanzia Mei 27 na yanatarajiwa kumalizika Juni 1.

Naibu katibu mkuu huyo akazitaka mamlaka za Serikali za mitaa kuwawezesha maafisa hao ugani waweze kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wafugaji katika kuhakikisha wanafunga kisasa na kuongeza uzalishaji.

"Maziwa yanayozalishwa hapa nchini yanachangia Kwa asilimia mbili kwenye pato la Taifa huku tasnia hiyo ya maziwa ikikua kwa asilimia 2.3," alisema Mtwale.

Awali akitoa taarifa ya maadhimisho hayo msajili wa bodi ya maziwa Tanzania Prof George Msalya alisema pamoja na kufanya kongamano na utoaji elimu kwa vikundi vya wafugaji na wasindikaji  wameweza kugawa maziwa kwa wanafunzi wa shule mbili za msingi katika Manispaa ya Morogoro.

Alisema kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kufungua fursa za kwenje tasnia ya maziwa kwa kutambua kuwa maziwa ni lishe na uchumi.

Baadhi ya wafugaji walieleza sababu za kuwepo Kwa uzalishaji mdogo wa maziwa lakini pia mwamko mdogo wa wananchi kunywa maziwa.

Katibu wa chama Cha wafugaji wilaya ya Kilosa Petro ole Melen alisema ni pamoja na mifugo duni inayotokana ana na mbegu za asili ambazo hazina uwezo wa kutoa maziwa ya kutosha, kukosekana kwa malisho na wafugaji wengi kukosa elimu ya ufugaji bora.

Alisema kama Serikali itatoa elimu kwa wafugaji itakayoendena na ugawaji wa mbegu bora za kisasa za mifugo mkoa wa Morogoro utaongeza uzalishaji wa maziwa na hivyo wananchi wataweza kunywa maziwa yaliyobora.

Mama wa kifugaji kutoka jamii ya kimaasai Kata ya Mikese Wilaya ya Morogoro Zawadi Baini aliiomba Serikali kuweka bei elekezi ya maziwa kama ilivyokuwa Kwa petrol kwani kukosekana kwa bei elekezi kunawafanya wauzaji na wazalishaji wa maziwa kupunjwa.

Akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Morogoro, mkuu wa wilaya ya Malinyi Sebastian Waryuba alisema 

Morogoro ni miongoni mwa mikoa yenye mifugo mingi ambayo sifa yake kubwa ni kusababisha migogoro hivyo inatakiwa kubadilishwa mtazamo.

Alisema tija ya uzalishaji wa maziwa ni ndogo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya teknolojia duni za ufugaji Elimu zaidi itolewe kwa wafugaji ili wafuge kisasa.

Waryuba alisema pamoja na uzalishaji huo wa maziwa kuwa mdogo lakini pia hata unywaji wa maziwa hapa nchini umekuwa chini ukilinganisha na nchi nyingine za Kenya na Uganda.