WATANZANIA WAHIMIZWA KUNYWA MAZIWA, BAADA YA KUACHA KUNYONYA
Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania Prof. George Msalya amesema kutokana na umuhimu na virutubisho vilivyopo kwenye maziwa, Watanzania wanatakiwa wanywe hata wanapoacha kunyonya ziwa la mama.
Amesema zaidi binadamu, wapo kundi moja la wanyama ambao wanategemea maziwa pale wanapozaliwa hadi wanapokua, ila changamoto inakuja wanapoacha kunyonya kwani wanashindwa kupangilia mlo kamili.
Msalya amesema hayo Agosti 12, 2024 wakati akichokoza mjadala kwenye Mwananchi X Space, inayoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) Tanzania pamoja na Taasisi ya Lishe na Chakula Tanzania (TFNC) wenye mada isemayo "Umuhimu wa kuwapa chakula mchanganyiko watoto wa shule"
"Tunakula vyakula vya namna moja kwa muda mrefu, mfano wali maharage na hali hiyo ipp hadi shuleni na hata sisi wakati tunasoma hatukuona maziwa wala nyama.
Mambo kama hayo yanasababisha hali ya lishe nchini kuwa duni," amesema Profesa na kuongeza kuwa maziwa ni chakula muhimu katika maisha ya mwanadamu.
"Ndio maana Mungu akaleta wanyama kama kondoo, mbuzi, ng'ombe, ngamia na punda ambao wanatoa maziwa kwa ajili ya kutumika kama mbadala, lakini changamoto inakuja ya uelewa watu wanapoacha kunyonya hawanywi tena maziwa bila kutambua wanaacha virutubisho muhimu," amesema.